Rwanda yazindua kampeni ya kuhimiza usawa wa kijinsia katika sekta ya afya
2023-09-06 14:11:53| cri

Rwanda imezindua kampeni inayolenga kuhimiza usawa wa kijinsia katika huduma za afya, hususan huduma ya afya ya akili. Kampeni hiyo itakayofanyika kwa mwaka mmoja inayoitwa “Sisi Wote ni Sawa” ni sehemu ya pendekezo la Shirikisho la Wake wa Marais wa Afrika kwa Maendeleo (OAFLAD), na inalenga kuongeza uelewa kuhusu afya ya akili na pia kuzuia au kugundua mapema magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika jumapili mjini Kigali, mji mkuu wa Rwanda, waziri wa nchi katika Wizara ya Afya nchini humo Yvan Butera, amesisitiza umuhimu wa afya ya akili, na kuongeza kuwa matatizo ya afya ya akili ni suala linaloweza kumpata mtu yoyote.

Maofisa wa afya wamesema baadhi ya watu wanatafuta tiba za jadi kutibu ugonjwa huo, wakati wengine hawapendi kutafuta huduma hospitali kutokana na fedheha au kukosa uelewa wa tatizo hilo.