Wawekezaji zaidi ya 100 wa China kushiriki kwenye Mkutano wa Jukwaa la Uwekezaji kati ya China na Tanzania
2023-09-06 09:13:10| CRI

Ujumbe wa wawekezaji zaidi ya 100 wa China umethibitisha kushiriki kwenye mkutano wa jukwaa la uwekezaji kati ya China na Tanzania utakaofanyika Septemba 25 kwenye kituo cha biashara cha Tanzania mjini Dar es Salaam.

Mkuu wa Eneo la Viwanda la Sinotan nchini Tanzania Bw. Huang Zaisheng, na mratibu wa jukwaa hilo amesema mkutano huo unaongozwa na ubalozi wa China nchini Tanzania na kuandaliwa kwa pamoja na Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania TIC, Mfuko wa Sekta Binafsi wa Tanzania TPSF na Shirikisho la Viwanda la Tanzania CTI.

Kwenye mkutano na wanahabari uliofanyika jumatatu huko Dar es Salaam, Bw. Huang amesema ujumbe wa China utakaoundwa na wajumbe zaidi ya 100 wa kiuchumi na kibiashara unaongozwa na kamati ya mkoa wa Zhejiang ya Baraza la Kuhimiza Biashara ya kimataifa la China na serikali ya mji wa Jinhua, Zhejiang.

Pia amesema kampuni za Jinhua, Zhejiang zinahusiana na sekta mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa dawa, mashine na vifaa, bidhaa za mahitaji ya kila siku nyumbani na huduma za usafirishaji, huku akiongeza kuwa wawekezaji wanalenga kuanzisha uhusiano wa kiwenzi wa muda mrefu na serikali na kampuni za Tanzania.