Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati atembelea Gabon
2023-09-06 09:20:28| CRI

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin Archange Touadera jana alipokelewa na rais wa mpito wa Gabon Brice Clotaire Oligui Nguema katika Ikulu ya Libreville nchini Gabon, lakini haijafahamika viongozi hao walijadili nini.

Rais Touadera ameteuliwa kuwa mpatanishi wa mchakato wa kidemokrasia nchini Gabon na mkutano maalumu wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (ECCAS) uliofanyika juzi baada ya mapinduzi ya kijeshi kutokea nchini Gabon.

Rais Nguema aliyeapishwa juzi baada ya kuongoza mapinduzi hayo aliahidi kuweka katiba mpya kwa mujibu wa kura za maoni, kanuni mpya za uchaguzi na adhabu na pia alisema “kurejesha haki kwa raia” na kufanya uchaguzi ulio “huru” na “wazi” baada ya kipindi cha mpito, lakini hakubainisha muda wa mpito huo.

Umoja wa Afrika umeisimamisha uanachama Gabon kutokana na mapinduzi hayo, hadi utaratibu wa kikatiba utakaporejeshwa nchini humo.