Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Utawala la Sudan latoa amri kuvunja Kikosi cha RSF
2023-09-07 09:02:00| CRI


 

Mwenyekiti wa baraza la Mpito la Utawala la Sudan na kamanda mkuu wa jeshi la Sudan Bw. Abdel Fattah Al-Burhan ametoa amri ya kikatiba kuvunja kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na baraza hilo, Bw. Al-Burhan ameamuru Kamandi Kuu ya Jeshi la Sudan, sekretarieti kuu ya baraza la utawala na mamlaka nyingine husika kutekeleza uamuzi huo.

Taarifa hiyo imesema uamuzi huo unatokana na athari za uasi wa kikosi hicho dhidi ya taifa, ukiukwaji mbaya uliofanywa nao dhidi ya raia wa kawaida, na hujuma kubwa dhidi ya miundombinu ya nchi hiyo. Licha na hayo, kikosi hicho pia kimekiuka malengo, majukumu na kanuni zilizo katika sheria kuhusu kikosi cha RSF iliyotolewa mwaka 2017.

Mwanzoni, kikosi cha RSF kilikuwa chini ya uongozi wa Idara ya Taifa ya Ujasusi na Usalama, baada ya hapo bunge la Sudan mwaka 2017 lilipitisha sheria ikifanya kikosi hicho kiongozwe na jeshi la nchi hiyo.