Mashirika ya kibinadamu nchini Sudan Kusini yalazimika kupunguza misaada kutokana na upungufu wa fedha
2023-09-07 08:47:44| CRI

Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini yamesema yanalazimika kupunguza mwitikio wa kibinadamu kwa mamilioni ya watu walio hatarini, kutokana na ukosefu wa fedha.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa mjini Juba, mashirika hayo yamesema kupungua kwa fedha kunawalazimisha kutoa kipaumbele kwa uungaji mkono muhimu wa kuokoa maisha, lakini hatua hiyo inahatarisha kuwaacha wengine mamilioni.

Kaimu mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nchini Sudan Kusini Bwana Makena Walker, amesema haya si maamuzi rahisi, na kipaumbele cha WFP ni kuokoa maisha ya watu wengi kadri iwezekanavyo, na kuongeza kuwa msaada wa dharura wa chakula uliisha mwezi Agosti katika maeneo mengi.