Mkutano wa kilele wa uwekezaji waanza nchini Rwanda ili kuendeleza ujenzi wa miji inayotumia teknolojia za kisasa barani Afrika
2023-09-07 08:48:18| CRI

Wajumbe wanaohudhuria Mkutano wa Uwekezaji wa miji ya Afrika inayotumia teknolojia za kisasa (Smart City) unaofanyika mjini Kigali, wametoa wito kwa viongozi na watunga sera wa Afrika kutetea kuundwa kwa miji inayotumia teknolojia za kisasa ili kupunguza msongamano, kuendeleza uvumbuzi na kukuza ukuaji endelevu wa miji.

Wajumbe wamesema hayo kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa siku tatu, ambao lengo lake ni kuangalia fursa za kuhimiza ukuaji endelevu, kuboresha maisha na kukuza uvumbuzi kote barani Afrika.

Meya wa mji wa Kigali Bwana Pudence Rubingisa amesema mustakbali wa miji ya kisasa uko mikononi mwao, lakini maendeleo ya miji hiyo yanategemea kujitolea kwao katika uvumbuzi na ushirikiano. Amesema kuna haja ya kuongeza uwekezaji katika kurahisisha usafiri, usimamizi wa taka na utoaji wa huduma wakati nchi zinapoanza kuendeleza miji ya kisasa.