China na Afrika zajenga jumuiya yenye hatma ya pamoja katika nyanja za amani na usalama
2023-09-07 15:10:23| CRI

Kongamano la tatu la Amani na Usalama kati ya China na Afrika lenye kauli mbiu ya “Utekelezaji wa Mpango wa Usalama wa Kimataifa, Kuimarisha Mshikamano na Ushirikiano kati ya China na Afrika” linafanyika mjini Beijng, na kuhudhuriwa na zaidi ya wajumbe 100 wakiwemo viongozi wa majeshi ya nchi za Afrika, maofisa waandamizi wa Umoja wa Afrika wanaoshughulikia mambo ya usalama, na mabalozi wadogo wa kijeshi wa nchi za Afrika nchini China.

Waziri wa Ulinzi wa China Li Shangfu kwenye kongamano hilo amesema wakati dunia imeingia katika kipindi kipya cha misukosuko na mabadiliko, huku binadamu akikabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa, China iko tayari kushirikiana na Afrika kuimarisha ushirikiano wao wa jadi wa urafiki na usalama. Amesema pande hizo mbili zitahimiza kwa pamoja utekelezaji wa Mpango wa Usalama wa Kimataifa katika ushirikiano kati ya China na Afrika ili kukabiliana na changamoto za kiusalama, sambamba na kulinda haki na uadilifu wa kimataifa, na kuangazia uhakika zaidi, amani na kuhimiza utu duniani.

Pia amesema China na Afrika zinapaswa kutekeleza kwa kina maafikiano muhimu yaliyofikiwa na viongozi wao, kuimarisha mawasiliano ya kimkakati na ushirikiano wa kivitendo, kuboresha zaidi ubora na ufanisi wa ushirikiano wa kiusalama, ili kutoa mchango mpya na mkubwa zaidi katika kudumisha usalama wa kikanda na kimataifa.

China na Afrika ni marafiki wakubwa na wenzi wazuri wanaosaidiana, na kutimiza amani na usalama wa kudumu ni matarajio ya pamoja ya watu wa China na Afrika. Katika suala hilo, China daima inaungana mkono na ndugu wa Afrika. Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya walinda amani wa China wametumwa barani Afrika, na hadi sasa zaidi ya askari 30,000 wa China wametekeleza majukumu katika maeneo 17 barani Afrika. China inaunga mkono nchi za Afrika kuimarisha utulivu na kuongeza uwezo wa kulinda amani, na kuunga mkono Afrika kutatua matatizo yake kwa njia za Kiafrika. China inatekeleza mapendekezo ya maendeleo ya kimataifa kwa hatua madhubuti, kuunganisha mipango yake ya maendeleo na mikakati ya maendeleo ya Afrika, ili kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya 2030, na kuhimiza usalama endelevu kupitia maendeleo endelevu.

Katika Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka jana, China na Afrika zilitangaza utekelezaji wa pamoja wa “Miradi Tisa”, ukiwemo mradi wa amani na usalama. Kwa mujibu wa mpango wa mradi huo, China itatekeleza miradi 10 ya ushirikiano katika nyanja ya amani na usalama, kuendelea kutekeleza usaidizi wa kijeshi kwa Umoja wa Afrika, kuunga mkono juhudi za nchi za Afrika za kudumisha usalama wa kikanda na kukabiliana na ugaidi, kutoa mafunzo, na kufanya ushirikiano wa udhibiti wa silaha nyepesi na vikosi vya kulinda amani vya China na Afrika.

Mafanikio ya kudumisha amani na usalama ndio msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ustawi wa watu barani Afrika, na yana umuhimu mkubwa kwa amani na maendeleo ya dunia nzima, ikiwemo China. China itashirikiana na Afrika kuzidisha ushirikiano katika nyanja ya amani na usalama, na kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja katika enzi mpya.