China yasaidia Afrika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi
2023-09-07 15:11:45| CRI

Mkutano wa kwanza wa kilele wa Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unafanyika huko Nairobi nchini Kenya. Katika miaka mingi iliyopita, China imechukua hatua madhubuti ili kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kutokana na mabadiliko ya tabianchi duniani, majanga kama vile ukame, mafuriko na mawimbi ya joto yametokea mara kwa mara barani Afrika, na kusababisha kuongezeka kwa jangwa, mmomonyoko wa ardhi, kutoweka kwa viumbe na ukosefu wa chakula. Wakati huohuo kiwango cha maendeleo ya uchumi barani humo bado ni chini, hivyo ni vigumu kwa Afrika kukabiliana na changamoto hizo peke yake.

China na nchi za Afrika zimeshirikiana vizuri kwa miaka mingi katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Kwa mfano katika kuhimiza matumizi ya nishati safi, ushirikiano kati ya pande hizo mbili umepata mafanikio mazuri. Katika miaka ya hivi karibuni, China imezisaidia nchi za Afrika kuendeleza matumizi ya nishati safi za jua, upepo, maji na jotoardhi kwa mujibu wa hali tofauti ya nchi zao, na kutekeleza miradi mingi mikubwa ya miundombinu ya nishati safi, ili kupunguza utoaji wa hewa inayoweza kuongeza joto na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Bwawa la Merowe nchini Sudan lenye urefu wa kilomita 9 limejengwa na kampuni ya China, na uwezo wake wa kuzalisha umeme unashika nafasi ya kwanza barani Afrika. Bwawa hilo limewanufaisha watu milioni 4 nchini Sudan, na kuboresha kwa kiasi kikubwa uwezo wa nchi hiyo katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Licha ya bwawa hilo, China pia imefanya miradi mingine mingi ya nishati mpya barani Afrika, ikiwemo Vituo vya Kuzalisha Umeme kwa Nishati ya Upepo vya De A nchini Afrika Kusini, Kituo cha Uzalishaji wa Umeme kwa Jotoardhi wa Okari nchini Kenya, na Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa Nishati ya Jua cha Photovoltaic nchini Ethiopia.

Kwa upande wa utafiti, wanasayansi wa China wanafanya mradi wa kimataifa wa utafiti kuhusu mabadiliko ya tabianchi, baadhi ya mada zao zinahusisha moja kwa moja na Afrika, kama vile athari ya mabadiliko ya tabianchi kwa maendeleo ya kilimo, rasilimali ya maji na usalama wa chakula katika Bonde la Mto Zambezi. Timu ya Utafiti wa Sayansi ya Mfumo wa Dunia ya Chuo Kikuu cha Tsinghua nchini China imeanzisha ushirikiano na nchi nyingi za Afrika, na miradi yake ni pamoja na uchoraji wa ramani ya rasilimali za misitu ya mianzi katika nchi tatu za Afrika Kusini zikiwemo Kenya, Uganda na Ethiopia, ili kutafiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa na jinsi ya kukabiliana nazo.

Mbali na ujenzi wa miundombinu ya nishati safi na utafiti wa kisayansi, ushirikiano kati ya China na Afrika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pia unahusisha ujenzi wa uwezo, na kuwafundisha wanasayansi vijana wa Afrika. Jambo ambalo lina umuhimu mkubwa sana kwa Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni, China imewapokea wanafunzi wengi kutoka nchi za Afrika kusoma sayansi ya asili nchini China, na wanafunzi hao watatumia ujuzi wao waliopata nchin China kusaidia Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.

Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa inayokabili binadamu wote duniani, na nchi yoyote haiwezi kushinda vita hii dhidi ya changamoto hiyo peke yake. China itaendelea kudumisha ushirikiano mzuri na nchi za Afrika ili kukabiliana na changamoto hiyo.