Raia wa Afrika Mashariki wakabiliwa na hali mbaya baada ya OPEC+ kupunguza uzalishaji wa mafuta
2023-09-08 14:45:18| cri

Wakazi na wafanyabiashara katika kanda ya Afrika Mashariki wanakabiliana na hali halisi ya kupanda kwa bei ya mafuta huku mamlaka ikirekebisha viwango hivyo ili kukabiliana na hali ya kimataifa.

Jumanne jioni, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ya Tanzania ilirekebisha bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa kwenda juu, ikipandisha lita moja ya dizeli kwa Sh324 huku ile ya petroli na mafuta ya taa ikipanda kwa Sh14 na Sh275, mtawalia. Chini ya bei hizo mpya zilizotangazwa, madereva wa Dar es Salaam sasa watalipa Sh3,213 kwa lita moja ya petroli, wakati lita moja ya dizeli itagharimu Sh3,259.

“Mabadiliko ya bei za mafuta ya petroli Septemba 2023 yamechangiwa zaidi na kupanda kwa bei katika soko la dunia kwa hadi asilimia 21, ongezeko la malipo ya uagizaji wa mafuta kutoka nje hadi asilimia 62, na siasa za kijiografia katika nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi (OPEC+),” Ewura ilisema Jumanne.

Na katika kile kinachoonekana kwamba changamoto hiyo inaweza kuwepo kwa muda mrefu, mafuta yalipanda zaidi katika soko la kimataifa juzi baada ya wazalishaji wakuu wa OPEC+ Urusi na Saudi Arabia kupunguza zaidi usambazaji hadi mwisho wa mwaka katika juhudi za kuongeza mapato yao.