Wapiganaji 107 wa al-Shabab wajisalimisha kwa serikali ya Somalia
2023-09-08 09:33:34| CRI

Kituo cha kukabiliana na ugaidi cha Somalia kimesema wapiganaji 107 wa kundi la al-Shabab wamejisalimisha kwa vikosi vya serikali ya Somalia kati ya mwezi Julai na Agosti.

Mkurugenzi wa kituo hicho Bw. Abdullahi Mohamed Nor, amesema wanamgambo hao walijisalimisha katika majimbo manne ya Hirshabelle, Galmudug, Kusini Magharibi na Jubaland.

Mkurugenzi huyo amewaambia wanahabari mjini Mogadishu kuwa waliojisalimisha ni pamoja na watoto wadogo, vijana, wanawake na makamanda wa vikundi ambao walikuwa na itikadi kali, na watapewa msamaha na kisha kupatiwa misaada ya kujiunga tena kwenye jamii.

Amewataka wapiganaji wa kundi hilo wenye lengo la kunufaika na msamaha wa serikali kuiga mfano huo, na watawakaribisha wakiondoka kutoka kwenye kundi la al-Shabab.