Benki za Kenya zazindua mfumo wa kuripoti mambo ya fedha ili kudhibiti hatari zinazotokana na tabia nchi
2023-09-08 09:04:57| CRI

Benki za Kenya zimezindua mfano wa namna ya kuripoti mambo ya kifedha unaohusiana na hatari za tabia nchi, ambao unatoa muhtasari wa jinsi wakopeshaji wa kibiashara wa nchi wanavyoweza kudhibiti hatari za kifedha zinazohusiana na mabadiliko ya tabia nchi.

Ofisa mkuu mtendaji wa Chama cha Mabenki cha Kenya (KBA) Bw. Habil Olaka, amesema mjini Nairobi kuwa mfano huo umejikitia kwenye nguzo nne zinazosimamia shughuli za benki, ikiwa ni pamoja na utawala, mkakati, usimamizi wa hatari na malengo.

Amesema benki zinaweza kuimarisha uwazi na kuwasilisha mbinu zao kuhusu hatari na fursa zinazohusiana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kenya ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazobeba mzigo mzito unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, ikishuhudia ukame mkali, matatizo ya maji na uhaba wa chakula.