China yapinga tuhuma za Marekani dhidi yake katika mkutano wa kilele wa Asia Mashariki
2023-09-08 15:45:45| CRI

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imepinga vikali tuhuma zilizotolewa na Marekani dhidi ya nchi hiyo katika Mkutano wa Kilele wa Asia Mashariki hapo jana, ambazo zinahusiana na suala la Taiwan na Bahari ya Kusini ya China.

Wizara hiyo imesisitiza kuwa, suala la Taiwan ni mambo ya ndani ya China ambayo hayatakiwi kuingiliwa na nchi za nje, na kwamba tishio kubwa kwa amani katika Mlango Bahari wa Taiwan linatokana na vitendo vya watu wa kisiwa hicho wanaodai ‘Taiwan kujitenga na China’ na uungaji mkono wanaopokea kutoka nje.

Wizara hiyo imeitaka Marekani kufuata kikamilifu kanuni ya China moja na taarifa tatu za pamoja za China na Marekani, kuacha kutumia suala la Taiwan kuingilia kati mambo ya ndani ya China, na kuchukua vitendo halisi kudumisha amani na utulivu wa mlango bahari wa Taiwan, na si kufanya vinginevyo.

Wizara hiyo pia imesema baadhi ya nchi zisizo za kikanda zinataka kuchochea machafuko, kuzusha makabiliano na kuhatarisha amani na utulivu katika Bahari ya Kusini ya China, na China daima imekuwa ikipinga hilo.