Kampuni ya teknolojia ya China yaunga mkono karakana mpya ya Luban nchini Kenya ili kuhimiza mafunzo ya ufundi stadi
2023-09-08 08:51:09| CRI

Kampuni ya teknolojia ya China Huawei imeunga mkono kuanzishwa kwa Karakana ya Luban katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Meru, iliyojengwa kwa pamoja na Chuo cha Ufundi Stadi cha Mji wa Tianjin kwa lengo la kushirikiana kwenye mipango ya maendeleo itakayopiga jeki mafunzo ya ufundi stadi nchini humo.

Adam Lane, mkurugenzi wa mahusiano ya serikali wa kampuni ya Huawei tawi la Kenya, amesema kupitia taarifa kuwa kampuni yake itatoa vifaa vya kisasa kwa Karakana ya Luban ili kuboresha mafunzo kwa wanafunzi.

Bw. Lane amesema Huawei inashirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Meru kuanzia mwaka 2019, na tayari imemaliza mafunzo kwa wahadhiri watano kuhusu akili bandia na usalama wa mtandaoni.