Mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu, mwimbaji maarufu wa nchini China, Coco Lee alifariki dunia kwa kujiua, na sababu iliyotajwa kuwa chanzo cha kifo chake, ni sonona, ama depression. Habari zinazema Coco Lee alikuwa na tatizo la muda mrefu la sonona, licha ya kuonekana kuwa mwenye furaha na mchangamfu. Inasemekana miaka kadhaa iliyopita, mwimbaji huyu alikumbwa na changamoto katika ndoa yake, na huo ndio ukawa mwanzo wa kuwa na msongo wa mawazo. Licha ya hayo, mwimbaji huu alijitahidi sana kutafuta tiba ya tatizo lake hilo, na akajikuta muda mwingi akijishughulisha Zaidi na kazi yake ya uanamuziki ili kujifurahisha.
Lakini kwa bahati mbaya, hali yake iliendelea kuwa mbaya Zaidi katika siku za karibuni, hivyo mama yake na dada zake wawili walijitahidi sana kumuunga mkono na kumsaidia bila kuchoka. Kifo cha mwimbaji huu kiliibua masuala mengi katika mtandao wa kijamii wa Weibo hapa China, ambapo watumiaji wa mtandao huo walikuwa na maswali mengi kuhusiana na sonona, na jinsi watu wenye tatizo hilo nchini China wanavyoficha hali zao ili kutoonekana tofauti na watu wengine. Katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake leo hii, tunazungumzia tatizo hili la sonona na jinsi linavyoathiri wanawake.