Jeshi la Sudan lakanusha kuua raia 40 katika soko la Khartoum
2023-09-11 10:48:05| CRI

Jeshi la Sudan (SAF) limekana kuhusika na mauaji ya raia 40 katika soko lililoko kusini mwa mji mkuu Khartoum.

Kamati ya upinzani ya Khartoum Kusini jana ilisema katika taarifa kwamba raia 40 waliuawa katika shambulizi la anga la ndege za kivita za SAF kwenye soko katika eneo la Mayo, kusini mwa Khartoum. Kamati hiyo pia ilichapisha picha zinazoonyesha idadi kubwa ya majeruhi na miili iliyofunikwa vitambaa.

Siku hiyo hiyo, Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) pia kilishutumu SAF kwa kuvamia vitongoji vya kiraia katika eneo la Mayo.

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya msemaji wake, SAF imekataa madai ya wanamgambo wa waasi ikisema kwamba ni ya upotoshaji na ya uwongo, na kubainisha kuwa haijawahi kulenga mkusanyiko wowote wa kiraia.

Kwa upande wake Shirika misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa limesema kwamba mapigano makali yaliyozuka kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF) nchini Sudan kuanzia katikati ya Aprili yamewalazimisha watu 259,451 kuingia Sudan Kusini. Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) ilionya kwamba watu wengi zaidi wanatarajiwa kuwasili wakati mapigano yakiendelea.