UNICEF yalalamikia ongezeko la vifo vya watoto kutokana na mabomu ya ardhini nchini Somalia
2023-09-11 10:46:44| CRI

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, limeeleza wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa vifo na majeraha makubwa kwa watoto waliokumbwa na milipuko ya mabomu ya ardhini ambayo imesababisha vifo vya watu 30 tangu mwezi Juni nchini Somalia.

Kaimu mwakilishi wa UNICEF nchini Somalia, Nejmudin Kedir Bilal, alisema watoto kadhaa wamekuwa wahanga katika matukio matatu tofauti yaliyohusisha mabomu ambayo awali hayakulipuka katika siku za hivi karibuni, na kubainisha kuwa nchi nzima, kwa uchache watoto wanne wanaripotiwa kufariki, na watano kupata majeraha ya kutishia maisha baada ya kucheza na mabaki ya mabomu hayo ya vita.

UNICEF imetoa wito kwa pande zote za mzozo nchini Somalia kukagua maeneo ya hatari mara kwa mara, kubeba jukumu la kushughulikia mabaki ya milipuko ya vita kwa uangalifu, na kuondoa mabomu yaliyopo na vifaa ambavyo havijalipuka.