Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limeeleza wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa milipuko ya mabomu yaliyotegwa ardhini yaliyosababisha vifo vya watoto 30 tangu mwezi Juni mwaka huu nchini Somalia.
Kaimu mwakilishi wa UNICEF nchini Somalia Nejmudin Kedir Bilal amesema, hivi karibuni, watoto wengi wamekuwa wahanga katika matukio matatu tofauti yaliyohusika na kulipuka kwa mabomu hayo.
Katika taarifa yake aliyoitoa mjini Mogadishu, Bw. Bilal amesema watoto wanne wameripotiwa kuuawa, na wengine watano kujeruhiwa vibaya baada ya kucheza na mabaki ya silaha za kivita.
UNICEF imetoa wito kwa pande zote husika za mapigano nchini Somalia kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa hatari, kuwajibika na kusimamia mabaki ya silaha za kivita kwa utaratibu maalum, na kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini yaliyopo sasa na vifaa vingine vyovyote vya mlipuko.