Tanzania yatarajia kuuza nyama Misri
2023-09-12 20:32:35| cri

Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Abdallah Ulega amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo wa Misri El Sayed El Kosayer ili kuona uwezekano na kuweka mazingira wezeshi ya biashara kwa nchi hizo, ikiwa ni jitihada za kufungua biashara hususani ya nyama inayotoka Tanzania kwenda Misri.

Pamoja na kujadiliana mambo mengine, suala la biashara ya nyama kutoka Tanzania kwenda kuuzwa nchini Misri lilijadiliwa kwa kina, huku Mhe. El Kosayer akiahidi kulifanyia kazi kwa haraka ili biashara hiyo iweze kuleta matunda kwa pande zote mbili.

Mapema wakati wa mazungumzo yao, Mhe. Kosayer alimueleza Waziri Ulega kuwa lengo la kukutana kwao ni kuona namna wanavyoweza kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi ili ziweze kuwanufaisha wananchi wa pande zote mbili.