Wabunge wa Tanzania wapongeza miradi ya BRI kwa kusaidia kufungua uchumi
2023-09-12 10:24:49| CRI

Wabunge wa Tanzania wamesema kuwa miradi inayotekelezwa chini ya Pendekezo la “Ukanda Mmoja Njia Moja” (BRI) inalisaidia taifa hilo la Afrika Mashariki kufungua uchumi wake.

Wabunge hao walitoa pongezi hizo Jumamosi walipotembelea miradi miwili mikubwa ya miundombinu inayotekelezwa na makampuni ya China katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga ikiwa ni sehemu ya mkakati wa BRI.

Wajumbe wa Kundi la Urafiki kati ya Wabunge wa Tanzania na China wametembelea eneo la ujenzi wa mradi wa Daraja la Magufuli katika Ziwa Victoria linalounganisha mikoa ya Mwanza na Geita unaotekelezwa na Kampuni ya Uhandisi na Ujenzi ya China (CCECC) pamoja na Shirika la 15 la Reli la China, na sehemu ya 5 ya reli ya SGR kutoka Isaka hadi Mwanza, unaotekelezwa na CCECC na Shirika la Reli la China (CRCC), kampuni mama ya Shirika la 15 la Reli la China.

Kiongozi wa Kundi la Urafiki wa Wabunge wa Tanzania na China, Geoffrey Mwambe, alisema miradi chini ya mfumo wa BRI inasaidia kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini humo, pia inazalisha ajira kwa wenyeji pamoja na kuhamisha teknolojia kwa wahandisi wa nchi hiyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya CCECC nchini Tanzania, Zhang Junle amesema ujenzi wa Daraja la Magufuli lililopewa jina la Rais wa zamani hayati John Pombe Magufuli umefikia asilimia 78 na kuongeza kuwa zaidi ya wahandisi wazawa 1,200 na wafanyakazi wenye ujuzi wameajiriwa kwa ajili ya mradi huu.