Mafuriko ya Mashariki mwa Libya yasababisha vifo vya zaidi ya watu 2,000
2023-09-12 10:23:07| CRI

Zaidi ya watu 2,000 wamefariki dunia na wengine maelfu kutojulikana walipo baada ya mafuriko kutokea Jumapili mashariki mwa Libya na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.

Akithibitisha maafa hayo ya mafuriko kupitia kituo kimoja cha televisheni nchini humo, waziri mkuu mwenye makazi yake mashariki mwa Libya, Osama Hammad, alisema, wahanga wengi waliripotiwa katika mji wa bandari wa Derna, ambapo "vitongoji vyote vilisombwa na mafuriko."

Alitoa wito kwa watumishi wa afya na timu za uokoaji nchini kote kutoa msaada kwenye mji huo ulioathirika zaidi, naye kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu wa Mashariki Ali al-Gatrani kupitia chaneli ya TV ya huko ameomba msaada wa kimataifa.

Mamlaka za eneo hilo zimetangaza siku tatu za maombolezo kwa wahanga.