Watu wasiopungua kumi wauawa kwenye shambulizi la mlipuko pwani ya Kenya
2023-09-12 10:19:03| CRI

Takriban wanajeshi kumi wameuawa katika shambulizi la mlipuko kando ya barabara katika kaunti ya Lamu, Pwani ya Kaskazini mwa Kenya.

Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) limelaani shambulizi hilo lililotokea siku ya Jumapili, lakini halikuthibitisha idadi kamili ya wahanga. Hata hivyo, ofisa mmoja wa usalama ambaye alikataa kutaja jina lake alisema wanajeshi kumi waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa baada ya gari lao lililokuwa likishika doria kukanyaga kilipuzi kilichokuwa kimetegwa kando ya barabara ya Milimani Baure.

Ofisa huyo alisema wafanyakazi kumi kati ya waliokuwa kwenye gari waliuawa papo hapo na wale waliopata majeraha wako katika hali mbaya.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu mjini Nairobi, KDF ilishutumu tukio hilo, ikisema wahalifu walikuwa wameazimia kuvuruga usafirishaji wa watu na bidhaa katika eneo hilo na hivyo kuharibu utulivu wa kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.