Rais wa Zanzibar aishukuru China kwa ushirikiano inaoutoa kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo
2023-09-12 10:29:29| CRI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru serikali ya China kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Tanzania ikiwemo Zanzibar kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo.

Dk. Mwinyi ametoa shukran hizo ikulu Zanzibar alipowakabidhi vyeti na medali timu ya madaktari 32 kutoka China waliohudumu kwenye hospitali za Zanzibar kwa kipindi cha mwaka mmoja, na kuwaaga baada ya kumaliza muda wao nchini humo.

Dk. Mwinyi amesema Zanzibar imenufaika na fursa nyingi kutoka China kupitia sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo Afya, hususan kupokea timu za madaktari bingwa wanaofika huko kubadilishana uzoefu na wazawa, hali aliyoielezea kuwa imeimarisha uhusiano mwema uliopo baina yao.

Kwa upande wake kiongozi mkuu wa timu ya madaktari hao 32, Dk. Zhao Xiaojun aliishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano ilioutoa katika kipindi chote, na kueleza kwamba Zanzibar ni visiwa vyenye upendo, amani na mshikamano kwa wenyeji na wageni.