Tume ya AU yaanza uchunguzi juu ya shambulizi lililotokea uwanja wa ndege nchini Somalia
2023-09-13 09:48:20| CRI

Tume ya mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) Jumanne ilisema imeanza kufanya uchunguzi juu ya jaribio lililofichuliwa la kukiuka kanuni za kiusalama katika lango la Madina, ambalo ni mojawapo ya malango makuu ya kuingia uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Mogadishu nchini Somalia.

ATMIS imesema tukio hilo lililotokea Jumapili linahusiana na mwanamume asiyejulikana, ambaye alijaribu kuingia kwenye kambi kuu ya ATMIS na ofisi za Umoja wa Mataifa bila ya kupitia ukaguzi wa lazima wa kiusalama. Baada ya askari kumtaka mtu huyo kukaguliwa alikataa na kumshambulia askari kwa kisu, hata hivyo askari mwingine alimuua mhalifu huyo.

ATMIS imewapongeza askari waliofanya operesheni ya haraka dhidi ya shambulizi hilo, na askari aliyejeruhiwa vibaya amepelekwa hospitali. ATMIS na vikosi vya usalama vya Somalia wanafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo.