Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la Dunia la Wafugaji Nyuki
2023-09-14 09:57:10| CRI

Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania Angellah Kairuki ametangaza kuwa nchi yake itakuwa mwenyeji wa Kongamano la 50 la Dunia la Wafugaji Nyuki ifikapo mwaka 2027.

Akiongea na wanahabari jijini Dar es Salaam Kairuki amesema kongamano hilo litakalofanyika katika jiji la Arusha kaskazini mwa Tanzania litavutia wajumbe zaidi ya 6,000 kutoka nchi mbalimbali duniani, na kwamba litaandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafugaji Nyuki (APIMONDIA) kwa kuwakutanisha wafugaji nyuki, wanasayansi, wafanyabiashara wa asali, mawakala wa maendeleo, mafundi na wabunge ili kusikiliza, kujadiliana na kujifunza kutoka kwa wenzao. Kairuki aliwataka wafugaji nyuki wa Tanzania kutumia kongamano hilo kukuza biashara ya ufugaji nyuki.

Kwa mujibu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, nchi hiyo inazalisha takriban tani 30,400 za asali kila mwaka, lakini mipango inaendelea ya kuongeza uzalishaji hadi tani 60,000 ifikapo mwaka 2025.