Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko nchini Libya yaongezeka hadi 5,500
2023-09-14 09:52:39| CRI

Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mafuriko makubwa yaliyopiga sehemu za mashariki mwa Libya imeongezeka hadi 5,500, na wengine 7,000 kujeruhiwa.

Msemaji wa huduma za dharura mjini Tripoli Osama Ali alisema kuwa hakuna idadi kamili ya vifo inayoweza kujulikana kwa sababu miili bado inaendelea kupatikana katika maeneo yaliyoathiriwa. Alisema kuwa takriban watu elfu kumi wameripotiwa kupotea na kwamba watu 30,000 wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na mafuriko hayo, na kuongeza kuwa mikoa iliyokumbwa na mafuriko inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vitu vya mahitaji ya kila siku.

Siku ya Jumapili, dhoruba ya Mediterania ilisababisha maporomoko ya udongo mashariki mwa Libya, na kusababisha mafuriko na uharibifu mkubwa wa miundombinu kwenye sehemu ilipopita dhoruba hiyo.