Uzalishaji wa dhahabu nchini Sudan wapungua kutokana na vita
2023-09-15 09:41:08| CRI

Kampuni ya taifa ya huduma za uchimbaji madini nchini Sudan imesema uzalishaji wake wa dhahabu umepungua hadi tani mbili kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Akithibisha hayo kwenye taarifa yake, msaidizi wa mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Rasilimali Madini ya Sudan, Miqdam Khalil Ibrahim, alisema jumla ya dhahabu zilizozalishwa na sekta za ushirika zilifikia tani mbili katika kipindi cha Aprili 15 hadi mwishoni mwa Agosti 2023 ikilinganishwa na tani 18 mwaka 2022. Alisema thamani ya dhahabu inayozalishwa imefikia dola za Marekani milioni 124, ambapo kati ya hizo serikali inapata dola milioni 25.5.

Usafirishaji wa dhahabu ni chanzo kikubwa cha fedha za kigeni cha Sudan. Mwaka jana Sudan ilisafirisha rasmi tani 34.5 za dhahabu zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 2. Kwa mujibu wa ripoti za awali za Umoja wa Mataifa, uchumi wa Sudan umeshuka kwa hadi asilimia 42 kutokana na mapigano yanayoendelea.