China yatoa wito kwa Shirika la Haki za Binadamu la UM kuzingatia suala la Japan kumwaga maji ya nyuklia baharini
2023-09-15 09:39:34| CRI

Mkuu wa Ujumbe wa China katika Umoja wa Mataifa huko Geneva Chen Xu, ametoa wito kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, kuzingatia zaidi suala la umwagaji maji taka ya nyuklia baharini la Japani na kuitaka nchi hiyo kuacha mara moja kitendo hiki.

Akizungumza na mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu za maji safi ya kunywa na usafi wa mazingira, Chen alisema kama maji yaliyochafuliwa na nyuklia ya Fukushima kweli ni salama, Japan isingelazimika kuyamwaga baharini, na kama si salama basi hakika Japan haifai kuyamwaga.

Chen alisema kuwa serikali ya Japani ilianza kumwaga maji yaliyochafuliwa na nyuklia kwa nguvu kutoka kwenye kinu cha nyuklia cha Fukushima kwenda baharini, hatua ambayo ilikiuka sana haki za afya, maendeleo na mazingira ya watu katika nchi za pwani ya Pasifiki na hata duniani kote.

Aidha amesisitiza kuwa, uhalali, haki na usalama wa umwagaji maji baharini umetiliwa shaka na jumuiya ya kimataifa na kupingwa vikali na watu wa Japan na Korea Kusini.