WHO yatangaza kutenga dola milioni mbili za kimarekani kwa ajili ya kuisaidia Libya
2023-09-15 09:46:18| CRI

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kutenga dola milioni mbili za kimarekani ili kuisaidia Libya iliyokumbwa na kimbunga na mafuriko.

Akizungumza na wanahabari kwenye makao makuu mjini Geneva, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Bw. Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema, kimbunga cha Daniel kilishambulia mashariki mwa Libya tarehe 10 na kupelekea mafuriko, ambayo yamesababisha vifo na majeruhi wengi, akiongeza kuwa haya ni maafa makubwa yasiyo na kifani. WHO itatenga dola milioni mbili za kimarekani kutoka mfuko wa kukabiliana na hali ya dharura ili kutoa msaada wa haraka katika sehemu zilizoathiriwa nchini Libya.

Tedros alisema vifaa vya matibabu na vitu vya tani 28 vitapelekwa katika sehemu zilizokumbwa na maafa nchini Libya tarehe 15. Aidha, WHO imeanzisha mtandao wa kikundi cha madaktari wa dharura.