Mkutano wa Kilele wa Kundi la Nchi 77 (G77) na China ulifanyika tarehe 15 na 16 Septemba huko mjini Havana, Cuba. Viongozi wa nchi za Latin Amerika waliohudhuria mkutano, wakiwemo rais Miguel Diaz-Canel Bermudez wa Cuba na rais Nicolas Maduro Moros wa Venezuela, walisisitiza kupigania haki sawa ya maendeleo na kupinga umwamba kando ya mkutano huo.
“Azimio la Havana” lililopitishwa kwenye mkutano huo wa kilele limesema kwa sasa changamoto inayoletwa na utaratibu usio wa haki juu ya uchumi wa kimataifa inaziathiri vibaya nchi zinazoendelea. Mageuzi yanahitaji kufanyika kwenye mfumo wa fedha ya kimataifa, nchi zinazoendelea zinapaswa kuimarisha mshikamano na ushirikiano, na kuongeza kiwango cha uwakilishi kwenye mashirika ya kimataifa yanayotoa maamuzi. Azimio hilo limesema pande zote husika zinapaswa kudhamiria kutimiza maendeleo ya dunia na ushirikiano wa kunufaishana kwenye msingi wa kujadiliana kwa pamoja, kujenga kwa pamoja na kunufaika kwa pamoja, na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.
Azimio hilo pia limesema sayansi, teknolojia na uvumbuzi vina umuhimu katika kuhimiza maendeleo endelevu kwa nchi zinazoendelea. Inapaswa kuimarisha Ushirikiano wa Kusini-Kaskazini na Kusini-Kusini, kuongeza uwezo wa nchi zinazoendelea katika kupata fursa za sayansi na teknolojia na kuendeleza sayansi na teknolojia, na kujenga mazingira ya maendeleo ya sayansi na teknolojia yenye uwazi, usawa, ushirikishi na yasiyo na ubaguzi.
Azimio hilo pia linapinga vikwazo vya upande mmoja dhidi ya nchi zinazoendelea.