UNESCO yaweka mandhari ya kitamaduni ya Gedeo ya nchini Ethiopia katika orodha ya urithi wa dunia
2023-09-18 08:39:26| CRI

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limeweka mandhari ya kitamaduni ya Gedeo ya nchini Ethiopia katika orodha yake ya urithi wa dunia.

Hatua hiyo imetangazwa jana mbele ya Waziri wa Utalii wa Ethiopia, Nasise Chale, katika mkutano wa 45 wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendelea mjini Riyadh, Saudi Arabia.

Waziri Chale amesema, eneo hilo la Gedeo linajumuisha msitu ambao umekuwa ukilindwa kizazi baada ya kizazi, ardhi yenye rutuba ya kilimo ambayo imekuwa ikitumiwa na watu wa huko wenye ujuzi wa jinsi ya kuhifadhi mfumo wa ikolojia na rutuba ya ardhi.

Eneo la Gedeo lilo katika ukingo wa mashariki wa Bonde Kuu la Ufa la nchini Ethiopia, katika uwanda wa juu wa nchini humo.