Wataalamu wa afya nchini Tanzania wataja vidokezo muhimu vya kusaidia kupambana na saratani
2023-09-18 10:56:21| cri

Wataalamu wa afya nchini Tanzania wametoa mapendekezo ambayo Tanzania inaweza kuyafuata ili kuharakisha mapambano dhidi ya saratani. Mapendekezo hayo ni pamoja na kuwa na njia mpya za kutambua saratani katika hatua za mwanzo.

Mapendekezo hayo yametolewa wakati ripoti ya hivi karibuni inaonesha kuwa Tanzania inapata hasara ya kiuchumi ya Sh2.8 bilioni kila mwaka kutokana na saratani. Ripoti iliyopewa jina la Saratani Kusini mwa Sahara na Tume ya Satarani ya Lancet ya 2020 inaonyesha kuwa saratani inaua wanawake zaidi kuliko wanaume, ambapo katika kila wanawake laki moja, 102 hufa, na kati ya kila wanaume laki 1 kuna vifo 82.

Mkurugenzi wa huduma za tiba katika Wizara ya Afya ya Tanzania, Prof. Paschal Ruggajo, amesema wanawake wanaathiriwa zaidi na saratani ya mlango wa kizazi na matiti, na takwimu zinaonesha kuwa katika kila wagonjwa wanne wanaogunduliwa kuwa na saratani, mmoja wao ana saratani ya shingo ya kizazi. Katika kila wagonjwa 10, mmoja ana saratani ya matiti. Saratani hizi mbili ni theluthi moja, sawa na asilimia 35.2, ya saratani zote zinazogunduliwa kwa wanawake.