Thamani ya uwekezaji nchini Tanzania yaongezeka kwa 120%, kilimo kinaongoza
2023-09-19 14:10:09| cri

Thamani ya uwekezaji nchini Tanzania katika muda wa mwezi mmoja uliopita imeongezeka kwa asilimia 120, huku sekta ya kilimo ikiendelea kuongoza kuwa sekta inayovutia zaidi uwekezaji.

Taarifa zilizotolewa hivi karibuni na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonyesha kuwa thamani ya miradi ya uwekezaji iliongezeka hadi kufikia Shilingi trilioni 2.33 kwa mwezi Agosti mwaka huu kutoka Shilingi trilioni 1.06 za mwezi Julai, idadi ya miradi pia iliongezeka hadi 58 kwa mwezi Agosti kutoka 40 mwezi Julai, na miradi hiyo 58 iliyosajiliwa mwezi Agosti inatarajiwa kuleta nafasi zaidi ya 25,700 za ajira.

Profesa Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo amesema takwimu hizo zinaonesha kuwa serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika maendeleo ya sekta ya kilimo, na kuongeza kuwa kuna kampeni kubwa zinazozingatia usalama wa chakula ambazo zitavutia uwekezaji zaidi katika sekta hiyo.