Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameonya juu ya vitendo vya dhuluma vinavyoendelea nchini Ethiopia, ikiwa ni karibu mwaka mmoja tangu kusimamishwa kwa mapigano kaskazini mwa nchi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Tume ya Wataalamu wa Haki za Binadamu kuhusu Ethiopia iliyoundwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Tume hiyo imesema ikiwa inakaribia mwaka mmoja tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusimamisha mapigano nchini Ethiopia, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu unaendelea kushuhudiwa nchini humo.
Mwenyekiti wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) Mohamed Chande Othman amesema, hali nchini Ethiopia bado ni mbaya, na kwamba makubaliano hayo yamewezesha kunyamazisha silaha, lakini hayajaleta suluhisho la mvutano katika sehemu ya kaskazini mwa Ethiopia, hususan mkoa wa Tigray, na pia hayajasaidia kuleta amani ya pande zote.