Watu 10 wauawa katika mapigano kati ya raia na jeshi nchini Sudan Kusini
2023-09-20 08:42:05| CRI

Jeshi la Sudan Kusini limesema, watu 10 wameuawa wakiwemo raia na maofisa usalama kufuatia mapigano ya siku mbili katika mji wa Pochalla, ulioko eneo la utawala la Greater Pibor, mashariki mwa nchi hiyo.

Msemaji wa Jeshi hilo Lul Ruai Koang ameliambia Shirika la Habari la China Xinhua, kwamba mapigano hayo yalianza jumapili baada ya jeshi kumsaka askari mmoja aliyekamatwa akiuza bunduki na risasi kutoroka mahabusu. Amesema ofisa huyo alijificha katika nyumba ya kamanda wake wa zamani.

Ameongeza kuwa, mapigano yalitokea jumapili jioni hadi jumatatu baada ya askari waliopelekwa kumkamata tena mtuhumiwa huyo kushambuliwa na vijana wa kabila la Anyuk waliokuwa na silaha wanaomuunga mkono kamanda huyo ambaye aliuawa kwenye mapigano hayo.