Kila sekunde 65, mtu hupata ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu maarufu kama ‘Alzheimer’. Kwa viwango vya sasa, wataalam wanaamini kwamba idadi ya watu wanaoishi na ugonjwa itaongezeka mara nne hadi kufikia mwaka 2050. Ugonjwa wa Alzheimer mara nyingi huitwa ugonjwa wa familia kwa sababu ya shinikizo la kudumu la kumwangalia mpendwa wako akipoteza akili zake polepole jambo ambalo humuathiri kila mtu.
Hivyo kila Septemba 21 ya kila mwaka, ni siku ambayo imetengwa kwa ajili ya ugonjwa huu ambapo mashirika ya Alzeima duniani kote huelekeza juhudi zao katika kuongeza ufahamu kuhusu Alzheimers na matatizo ya akili. Ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu ndio aina ya kawaida ya tatizo la akili, kati ya magonjwa yanayoathiri utendaji wa akili.
Siku ya Alzheimer Duniani ni fursa nzuri kwetu ya kupaza sauti zetu na kutafuta njia mpya za kupambana na athari za ugonjwa huo. Na katika kipindi cha leo cha ukumbi wa Wanawake tutaangalia tatizo hili la ugonjwa wa Alzheimer ambao unaonekana kuathiri zaidi wanawake.