Wakati wa wiki ya Mkutano wa 78 wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mkutano wa Kilele wa Matarajio ya Hali ya Hewa wa 2023 ulifanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. Kwenye hotuba yake kwa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres kwa mara nyingine tena amezitaka nchi wanachama ziharakishe juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kubadilisha mipango iwe hatua halisi.
Katika hotuba yake, Bw. Guterres amesisitiza kuwa lengo kuu kwa sasa ni kupata ufumbuzi kuhusu changamoto hiyo. Ameongeza kuwa hali mbaya ya hewa kama vile joto kali na mafuriko vimeleta maafa makubwa kwa binadamu. Ikiwa hakuna mabadiliko yoyote yatakayofanywa, joto duniani litapanda kwa nyuzi 2.8, na dunia itaelekea kwenye hatari na ukosefu wa utulivu. Amesema hili linahitaji hatua halisi kutoka kwa viongozi wa mataifa kwenye nyanja za kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa, kuhama kutoka matumizi ya nishati ya visukuku hadi nishati endelevu, kulinda haki ya tabianchi, na kuhimiza mfumo wa kifedha wa kimataifa uunge mkono hatua za tabianchi.
Bw. Guterres pia amesema mkutano mmoja wa kilele hautabadilisha dunia, lakini ni wakati wenye nguvu wa kuleta msukumo. Nchi wanachama lazima ziharakishe juhudi, zibadilishe mipango kuwa vitendo, na kugeuza mwelekeo wa mabadiliko ya tabianchi.