Afrika yapaswa kuharakisha kuongeza uwezo wa uzalishaji wa chanjo wa ndani
2023-09-21 08:35:32| cri

Makamu wa Rais wa Afrika Kusini Bw. Paul Mashatile amesema Afrika inapaswa kuharakisha kuongeza uwezo wa uzalishaji wa chanjo kwa kujitegemea na uwezo wa kuzuia majanga kupitia ushirikiano wa kimataifa.

Bw. Mashatile amesema hayo wiki hii mjini Cape Town, na kuongeza kuwa, wakati janga la COVID-19 lilipotokea, Afrika, kama maeneo mengine, ilikumbana na changamoto kubwa katika kupata chanjo za kutosha. Amesema katika dunia inayoendelea kubadilika, nchi za Afrika hazipaswi kuendelea kupata chanjo na uwezo wa kukabiliana na majanga kwa kutegemea nguvu za nje.

Pia amesema, kupitia mpango wa Wenzi wa Uzalishaji wa Chanjo wa Afrika unaoratibiwa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika, bara hilo limechukua hatua madhubuti katika kujitosheleza kwa uzalishaji wa chanjo, lengo likiwa ni kuzalisha asilimia 60 ya jumla ya chanjo zinazohitajika na bara la Afrika itakapofika mwaka 2040.