Wataalamu wa kilimo wa China waanzisha mafunzo ya teknolojia nchini Kenya
2023-09-21 08:51:24| CRI

Chuo Kikuu cha Kilimo cha Nanjing cha China na Chuo Kikuu cha Egerton cha Kenya vimeandaa kwa pamoja semina ya wiki moja kuanzia jumatatu wiki hii, kuhusu uendelezaji wa kilimo kati ya China na Afrika na uzalishaji wa nyanya katika vijiji vya mfano vya upunguzaji wa umaskini.

Semina hiyo imewashirikisha maofisa wa kilimo, wakulima, wafanyakazi wa makampuni na wanafunzi. Washiriki kutoka Kenya wamesema ushirikiano na wataalamu wa China utawanufaisha wakulima wa eneo hilo, na kutarajia kuwa teknolojia mpya zitazidi kuwasaidia wakulima kuongeza mapato. Pia wamesema, nyanya ni zao muhimu la kilimo katika Kaunti ya Nakuru nchini Kenya, na mafunzo hayo yatawawezesha kujifunza teknolojia za hali ya juu ambazo zinaweza kuchangia ongezeko la mapato ya wakulima na kutatua matatizo ya usalama wa chakula.

Naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Egerton Richard Mulwa amesema chuo hicho kimefanya ushirikiano wa muda mrefu na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Nanjing, na wataalamu wa kilimo wa China wametoa msaada halisi kwa watu wa eneo hilo, ili kuwasaidia wakulima kuongeza mavuno ya mazao na kuleta faida nzuri za kiuchumi.