Umoja wa Mataifa waonya kuwa mgogoro wa Sudan unaweza kuwa janga la kibinadamu
2023-09-22 08:40:37| CRI

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu, Martin Griffiths ameonya kuwa, kuruhusu mapigano nchini Sudan kuwa vita kamili ya wenyewe kwa wenyewe inaweza kuwa janga kubwa la kibinadamu.

Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Sudan kando ya Baraza Kuu la 78 la Umoja wa Mataifa, Bw. Griffiths amesema mapigano nchini Sudan yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 5,000, wengine zaidi ya 12,000 kujeruhiwa, na watu wengine zaidi ya milioni tano kukimbia makazi yao, wakiwemo watu zaidi ya milioni moja waliolazimika kukimbilia nchi jirani.

Pia amesema, mfumo wa afya nchini Sudan umevurugika, huku asilimia karibu 80 ya husuma za afya hazifanyi kazi na zaidi ya watu milioni 6 wanakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula.

Mkutano huo uliitishwa na Misri, Saudi Arabia, Qatar, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu Masuala ya Kibinadamu.