China yatoa waraka kuhusu jamii ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja
2023-09-26 14:38:34| cri

Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali la China imetoa waraka unaoitwa “Jamii ya Binadamu Yenye Mustakabali wa Pamoja: Mapendekezo na Hatua za China.”

Kwa mujibu wa waraka huo, miaka kumi iliyopita, Rais Xi Jinping wa China alitoa pendekezo la kujenga jamii ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja, ambalo lilitoa nuru wakati dunia ilipokuwa ikikabiliwa na hali ya sintofahamu, na kuwakilisha mchango wa China katika juhudi za kimataifa za kulinda dunia na kujenga siku za baadaye zilizo nzuri na ustawi wa pamoja.

Waraka huo umesema, ili kujenga jamii yenye mustakabali wa pamoja, binadamu wote, nchi zote, na kila mtu ni lazima kusimama pamoja katika shida na raha, na kusonga mbele kwa masikilizano zaidi katika dunia tunayoishi.

Waraka huo umetoa wito kwa juhudi zaidi katika kujenga dunia ya uwazi, jumuishi na nzuri itakayokuwa na amani ya kudumu, usalama kwa wote, na ustawi wa pamoja, na kufanya kweli haja ya watu ya kuwa na maisha bora.