Msukosuko wa kiafya wa Sudan wazidi kuwa na changamoto zaidi
2023-09-28 08:59:13| CRI

Wasiwasi unazidi kuongezeka kutokana na hali mbaya ya kiafya ya Sudan, huku kukiwa na ongezeko la magonjwa ya milipuko ya msimu, pamoja na mgogoro unaoendelea kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Wizara ya Afya ya Sudan imekiri kutokea kwa maambukizi ya homa ya dengue, malaria, na kipindupindu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Kwenye taarifa iliyotolewa kwenye ukurasa wake wa Facebook, wizara hiyo imeripoti vifo 21 vinavyohusiana na kipindupindu katika majimbo ya Khartoum na Gedaref. Taarifa pia imesema watu 265 wanadhaniwa kuambukizwa kipindupindu katika Jimbo la Gedaref, na 18 wamekufa kwa ugonjwa huo, watu 13 wameambukizwa katika jimbo la Khartoum, na watatu kati yao wamekufa.

Kaimu waziri wa afya wa Sudan Bw. Haitham Mohamed lbrahim amesema homa ya dengue inaenea katika majimbo 8 ya Bahari Nyekundu, Kassala, Gedaref, Gezira, Sinnar, Kordofan Kaskazini, Kordofan Kusini na Darfur Kaskazini.