IGAD yaonya kuongezeka kwa joto pamoja na mvua za El Nino katika kanda ya Afrika Mashariki
2023-09-28 14:11:59| cri

Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa (ICPAC) kilicho chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) kimesema nchi za Pembe ya Afrika, ambazo ni pamoja na Kenya, Somalia na Ethiopia, zitashuhudia hali ya joto kali zaidi ya kawaida kati ya mwezi Oktoba mpaka Desemba, kipindi ambacho kanda hiyo pia inatarajiwa kuwa na mvua za El Nino zitakazosababisha mafuriko makubwa.

Katika ripoti yake mpya ya utabiri wa hali ya hewa iliyotolewa mjini Nairobi, Kenya, hapo jana, ICPAC imesema baadhi ya nchi katika Pembe ya Afrika zitakuwa na ongezeko kubwa la joto, ambalo linaweza kufikia nyuzijoto 40 wakati baadhi ya nchi katika kanda hiyo zikikabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti hiyo pia imesema hali ya joto kali inaweza kushuhudiwa katika baadhi ya sehemu za nchini Ethiopia, kusini mwa Uganda, Rwanda, Burundi, na baadhi ya maeneo ya nchini Tanzania.