Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la wasichana wenye umri mdogo kutumia dawa za uzazi wa mpango. Wasichana hao wenye umri wa chini ya miaka 18, wanatumia dawa hizo bila kufuata ushauri wa daktari, na pia kutofahamu madhara ya matumizi ya dawa hizo kwa muda mrefu. Kinachoshangaza ama kusikitisha ni kwamba, wazazi, na/au walezi wa watoto hao wa kike wanaruhusu jambo hilo kwa kuhofia mimba za utotoni. Wataalamu wanasema matumizi ya muda mrefu wa dawa za uzazi wa mpango yanaweza kuwa na athari kubwa kwa mtumiaji, na kumsababishia magonjwa mengi ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi.
Jambo lingine linaloongeza matumizi ya dawa hizi, hususan dawa ya P2 ambayo inapaswa kutumika pale mwanamke ama msichana amejamiiana katika siku za hatari, ama amebakwa, ni kwamba wasichana wanaichukulia kama njia rahisi ya kukwepa hatari ya kupata mimba. Katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake leo hii tunazungumzia athari za matumizi ya dawa za uzazi wa mpango bila ya kufuata ushauri ama maelekezo ya wataalamu wa afya.