Wateja wa bandari ya Mombasa walia na ushuru 'haramu'
2023-09-30 22:32:47| cri
Watumiaji wa bandari ya Mombasa wana wasiwasi kwamba kukithiri kwa kanuni za baharini zinazowekwa na baadhi ya makampuni ya meli wakishirikiana na maafisa wa bandari kunaweka hatarini msimamo wa bandari kama lango kuu la Afrika Mashariki na Kati.
Wanadai kuwa baadhi ya makampuni ya meli yanaingiza tozo kiholela bila idhini ya Mamlaka ya Usafiri wa Baharini (KMA), ambapo baadhi yao yanatoza hadi dola 1,200 kwa kontena la futi 40, zaidi ya ule unaotozwa na bandari ya Dar es Salaam ya Tanzania.
Suala hili limekuwa likilaumiwa na wateja wengi, na kusababisha kupungua kwa usafirishaji wa shehena nchini Kenya. Shehena zilizohudumiwa kupitia Mombasa zilipungua kutoka tani milioni 34.6 mwaka 2021 hadi asilimia 1.9 ambayo ni tani milioni 33.9 mwaka 2022, licha ya msongamano wa makontena ya futi 20 kuongezeka kidogo hadi tani milioni 1.45.