Waziri wa Uturuki asema "magaidi" ndio walisababisha mlipuko wa Ankara
2023-10-02 08:41:13| CRI

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya amesema mlipuko uliotokea Jumapili karibu na Wizara ya Mambo ya Ndani ulisababishwa na "magaidi" waliojaribu kufanya shambulizi la bomu.

Akifafanua kuhusu mlipuko huo kwenye mtandao wa kijamii wa X, zamani ukijulikana kama Twitter waziri Yerlikaya alisema kuwa magaidi wawili walikwenda na gari mbele ya lango la kuingilia katika Kurugenzi Kuu ya Usalama ya Wizara ya Mambo ya Ndani na kufanya shambulio la bomu, ambapo maafisa wawili wa polisi walijeruhiwa kidogo, na mmoja wa magaidi hao alijilipua na gaidi mwingine kudhibitiwa.

Shambulio hilo lilitokea karibu na bunge la Uturuki, lililotazamiwa kukutana tena Jumapili baada ya mapumziko ya majira ya joto, ambapo Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alipangiwa kutoa hotuba.