Benki Kuu ya Dunia na Rwanda washerehekea miaka 60 ya ushirikiano imara
2023-10-02 08:45:30| CRI

Benki Kuu ya Dunia na serikali ya Rwanda Ijumaa walisherehekea kumbukumbu ya miaka 60 ya ushirikiano wao uliozaa matunda.

Akiongea kwenye sherehe hiyo Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Kenya, Rwanda, Somalia na Uganda, Keith Hansen, alisema ushirikiano wao thabiti na Rwanda ulianza miaka 60 iliyopita wakati nchi hiyo ilipokuwa mwanachama wa Benki ya Kimataifa ya Ujenzi na Maendeleo na Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa.

Alifafanua kuwa katika miaka hiyo, Benki ya Dunia imefadhili uwekezaji na kuendesha shughuli katika sekta mbalimbali, zikiwemo rasilimali watu, miundombinu, ustahimilivu wa kilimo, na maendeleo ya sekta binafsi, kwa jumla ya dola za Kimarekani bilioni 8.2, na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Rwanda. Ameongeza kuwa Rwanda inaonesha hadithi ya kupunguza umaskini na kuleta maendeleo.

Kwa upande wake waziri wa fedha na mipango ya kiuchumi wa Rwanda Uzziel Ndagijimana, alisema katika hafla hiyo kwamba serikali ya Rwanda inatambua jukumu lisiloyumba la Benki ya Dunia katika kusaidia mwelekeo wa maendeleo wa nchi hiyo katika miongo sita iliyopita.