Rais wa Tanzania azindua tovuti ya hifadhi ya nyaraka ya Salim Ahmed Salim
2023-10-02 08:40:37| CRI

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Jumamosi alizindua Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka ya Dk. Salim Ahmed Salim, inayolenga kuhifadhi urithi wa uongozi wa mwanadiplomasia mashuhuri wa kimataifa kwa njia ya kidijitali.

Akizindua tovuti hiyo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, Samia alimtaja Salim kama kiongozi aliyefanya kazi kwa bidii, nidhamu na kujali muda. Mkuu huyo wa nchi alitoa wito kwa viongozi na wananchi wa Tanzania kuingia kwenye tovuti hiyo ya hifadhi ya nyaraka na kujifunza kile ambacho Salim alifanikisha katika ngazi za ndani na kimataifa.

Alisema tovuti hiyo ina mkusanyo wa video, picha na maandishi, zikiwemo hotuba na nyaraka za kitaaluma za Salim, aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania, mwakilishi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa, Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa Umoja wa OAU kuanzia mwaka 1989 hadi 2001.

Septemba 2019, serikali ya China ilimtunuku Salim nishani ya juu ya kitaifa “Nishani ya Urafiki”, kwa kutambua mchango wake katika kuhakikisha China inapewa kiti chake kwenye Umoja wa Mataifa mwaka 1971 alipokuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye UM.