Afisa wa Tume ya AU atoa wito wa kuhakikisha maendeleo jumuishi kwa raia wa Afrika
2023-10-03 08:44:50| CRI

Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Monique Nsanzabaganwa ametoa wito wa kuhakikisha maendeleo jumuishi kwa raia wa Afrika.

Afisa huyo mkuu wa AU alisema hayo wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la AU, ambao unafanyika Oktoba 1-3 mjini Kigali, Rwanda, chini ya kaulimbiu ya "Kuharakisha Utekelezaji wa Ajenda ya 2063".

Alieleza kuwa wakati wanafuatilia dira ya kuwa na sauti sawa katika maamuzi ya kimataifa, pia wanapaswa kuhakikisha kwamba hakuna raia wa nchi za Afrika anayeachwa nyuma katika shughuli za maendeleo, iwe katika ngazi ya serikali za mitaa, kitaifa au bara.

Nsanzabaganwa alisisitiza umuhimu wa kutambua mwongozo wa maendeleo ya bara la Afrika wa miaka 50, Agenda ya 2063, kuelekea kufikia maendeleo jumuishi ya Afrika. Rasimu ya mpango wa pili wa utekelezaji wa miaka 10 iliangazia mambo saba ambayo yanawiana na kila moja ya matarajio saba ya Ajenda ya 2063, ambayo kwa uchache ni pamoja na kuona Afrika iliyounganishwa na kushikamana zaidi, taasisi za umma ziitikie zaidi mahitaji ya wananchi na Afrika kutatua migogoro kwa njia ya amani.