Zaidi ya watoto 300,000 wa Tanzania waokolewa katika mazingira yasiyo salama
2023-10-04 08:45:12| CRI

Serikali ya Tanzania imeokoa takriban watoto 335,971 katika mazingira yasiyo salama, ikiwa ni pamoja na aina mbaya zaidi za utumikishwaji wa watoto, biashara haramu ya binadamu na ukatili dhidi ya watoto, kati ya Julai 2022 na Aprili 2023.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Nandera Mhando, ambapo aliongeza kuwa kati ya watoto waliookolewa, wasichana ni 167,337 na wavulana 168,634.

Akibainisha kuwa watoto hao walifanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kila aina, vikiwemo ajira za watoto, ukatili, mazingira duni ya usafi na biashara ya binadamu, Mhando alisema watoto hao waliokolewa baada ya kutambuliwa na mamlaka za serikali za mitaa nchini kote.

Mhando alisema watoto hao waliookolewa hivi sasa wanaishi katika vituo 344 vya watoto vinavyosimamiwa na serikali kote nchini na baadhi yao wanaishi na ndugu zao, na kuongeza kuwa vituo hivyo vinawapatia mahitaji muhimu ikiwemo chakula, mavazi na elimu.