Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric Jumanne alisema, walinzi wa amani wa UM na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameanza operesheni dhidi ya kundi lenye silaha la CODECO huko Djugu, mkoani Ituri.
Dujarric alisema operesheni hiyo imefanyika ili kujibu mashambulizi dhidi ya raia yaliyotokea katika siku za karibuni na uwepo wa waasi wa kundi la CODECO walioko katika eneo hilo.
Kabla ya operesheni hiyo ya pamoja, serikali ya DRC imetaka tume ya kulinda amani ya UM nchini DRC (MONUSCO) iondoke nchini humo. Rais Felix Tshisekedi wa DRC alitoa agizo mwezi uliopita akitaka MONUSCO iondoke ndani ya mwaka huu. Sababu ni kuwa walinzi wa amani hawakuwalinda watu wanaolengwa na makundi ya waasi.
Dujarric alisema ripoti za karibuni kabisa zinaonesha kuwa vikosi vya CODECO viko karibu na kambi ya wakimbizi ya Lala, takriban kilomita 9 kusini mashariki mwa Djugu. Walinzi wa amani wanaendelea kufanya msako kwenye eneo hilo, ili kuwalinda raia na kuzuia makundi yenye silaha.